Uhusiano bora kati ya serikali ya taifa na zile za kaunti, umetajwa kuwa nguzo muhimu katika kufanikisha ugatuzi hapa nchini.
Hayo yalisemwa na katibu katika wizara ya kilimo Dkt. Kiprono Rono, katika kongamano lililowaleta pamoja wadau wa kilimo katika kaunti ya Mombasa.
Mkutano huo ambao lengo lake kuu ni kuimarisha sekta ya kilimo hapa nchini, uliafikia maazimio 17 ya kupiga jeki sekta hiyo muhimu ambayo imetajwa kuwa uti wa mgongo wa taifa hili.
Maazimio hayo ni pamoja na kuimarisha mpango wa kuhifadhi maziwa, kubuni sera ya taifa kuhusu ugavi wa ardhi ya kilimo, kuboresha ufuatiliaji wa mifugo, kuwiainisha uhamishaji wa rasilimali za ugatuzi wa kilimo na kubuni mkakati kuhusu usambazaji wa takwimu.
Kulingana na Dkt. Rono ushirikiano huo ni muhimu kwa ubadilishanaji wa mawazo na utaharakisha mpango wa kuimarisha uchumi wa taifa hili kuanzia chini almaarufu Bottom up Economic Transformational Agenda (BETA), unaolenga kushughulikia changamoto katika sekta ya kilimo na kutimiza utoshelevu wa chakula.
Waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na waziri wa Kilimo Dkt. Andrew Karanja, katibu katika idara ya ustawishaji mifugo Jonathan Mueke, mwenyekiti wa baraza la Magavana Abdullahi Ahmed na naibu mweneyekiti wa baraza la Magavana Mutahi Kahiga, miongoni mwa maafisa wengine wa ngazi za juu.