Dkt Karanja: Ipo haja kukumbatia huduma za nyanjani za kilimo kidijitali

Tom Mathinji
2 Min Read
Waziri wa kilimo Dkt. Andrew Karanja. apigia debe huduma za nyanjani za kilimo.

Huduma za nyanjani za kilimo ni muhimu sana katika kuhakikisha utoshelevu wa chakula, asema waziri wa kilimo na ustawi wa mifugo Dkt. Andrew Karanja.

Kulingana na waziri huyo, maafisa wa kutoa huduma za nyanjani za kilimo huwapa wakulima ujuzi unaohitajika kwa lengo la kuhahikisha  kilimo endelevu,

Dkt. Karanja, aliyasema hayo jana Alhamisi alipozindua kongamano kuhusu utoaji huduma za ushauri wa kilimo (KeFAAS).

Waziri huyo alisisitiza kuwa ufanisi wa mabadiliko katika sekta ya kilimo, utasababishwa na kuwepo kwa huduma za nyanjani za kilimo.

Aidha Dkt. Karanja alidokeza kuwa sekta ya kilimo ni kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi wa taifa hili, kwa kuwa hubuni nafasi za ajira na kuchangia katika ukuaji wa maeneo ya mashinani.

Ili kufanyia mabadiliko sekta ya kilimo, waziri Karanja alisema huduma za nyanjani ni sharti zikumbatiwe, hasaa katika viwango vya kaunti kwa kuwahusisha vijana walio na ujuzi wa kidijitali.

“Wizara ya kilimo inashirikiana na serikali za kaunti, sekta ya kibinafsi na wadau wote kufanyia sekta ya kilimo mabadiliko ili iwe bunifu zaidi na inayotekelezwa kibiashara. Juhudi zinafanywa kuimarisha utoaji wa huduma za kilimo za nyanjani,” alisema waziri huyo.

Alirejelea kujitolea kwa wizara yake kuendelea kushirikiana na wadau wote kuhakikisha utoshelevu wa chakula, huku wakulima wakiendelea kufaidika.

Share This Article