Mwaka mmoja tangu kuanzishwa, mpango wa lishe shuleni kwa jina “Dishi na County” umefanikiwa pakubwa huku ukigusa maisha ya wengi katika kaunti ya Nairobi.
Kulingana na takwimu zilizotolewa na serikali ya kaunti ya Nairobi, watoto zaidi ya laki tatu wanaosomea shule za umma za kaunti ya Nairobi wananufaika.
Idadi hiyo inajumuisha wanafunzi wote wa shule za umma katika kaunti ya Nairobi ambao hulipa shilingi tano tu kwa siku ili kupata mlo.
Kando na kufaidi wanafunzi, mpango wa Dishi na County umetoa nafasi za ajira zaidi ya elfu 2, ambazo ni za wapishi, wanaopakua, madereva wa malori ya kusambaza chakula, wajenzi wa jikoni na hata wakulima wadogo wanaouzia mpango huo chakula ambacho hupikwa.
Kwa sasa, wanafunzi wanapatiwa wali kwa maharagwe au wali kwa ndengu, huku Gavana Sakaja akiahidi kwamba aina za vyakula wanavyotoa itaongezeka katika siku zijazo.
Akihutubia wanahabari katika hoteli moja jijini Nairobi, Gavana Sakaja alidhihirisha furaha yake kwamba mpango huo alioanzisha umefanikiwa akiwa na imani kwamba utakuwa mkubwa zaidi siku za usoni.
Dhamira ni kuhusisha shule za kibinafsi ambazo zinasuasua katika utoaji wa lishe kwa wanafunzi ili kuhakikisha wanadumishwa shuleni wakati wote.
Gavana huyo alisimulia kisa cha mwanafunzi mmoja ambaye alikuwa yatima aliyefaidika na mpango huo na ambaye matokeo yake yaliboreka kiasi cha kufanya vyema kwenye mtihani wa kitaifa na akajiunga na shule ya upili ya kitaifa.
Alizungumza pia kuhusu mama aliyefahamu kupitia kwa mwanawe ujio wa mpango huo na akapata ajira katika ujenzi wa jikoni na sasa anahudumu kama mmoja wa wapishi.
Mpango huo ulianzishwa rasmi Agosti 28, 2024 baada ya ujenzi wa haraka wa jikoni 10 ambapo chakula huandaliwa na kusambazwa kwa shule zilizo karibu.
Jikoni hizo 10 zilijengwa katika muda wa miezi 10 pekee na kuna nyingine 7 zinaendelea kujengwa lengo likiwa kuhakikisha kila eneo bunge la kaunti ya Nairobi linakuwa na jikoni moja.