Dimba la Ulaya kurejea kwa duru ya pili leo

Dismas Otuke
1 Min Read

Kindumbwendumbwe cha kuwania kombe la bara Ulaya, mfumo mpya hatua ya makundi, kitarejea leo kwa mechi 9 huku nyingine tisa zikisakatwa kesho.

Arsenal waliotoka sare katika mkwangurano wa ufunguzi ugenini Atalanta, watakuwa nyumbani kuwaalika mabingwa wa Ufaransa Paris St. Germain.

Mabingwa wa Uingereza Manches City walioambulia sare tasa dhidi ya Inter Milan ya Italia nyumbani, watakuwa ugenini dhidi ya limbukeni Slovan Bratislava ya Slovakia.

Barcelona kutoka Uhispania watawatumbuiza Young Boys kutoka Uswizi, Redbull Salzburg ya Austria iwe nyumbani dhidi ya Brest Stade Brestois 29 ya Ufaransa, huku VfB Stuttgart ya Ujerumani ikimenyana na Sparta Praha ya Jamhuri ya Czech.

FK Crvena Zveda ya Serbia watakuwa na mtihani mgumu wakiwazuru Inter Milan nao Borusia Dortmund wawe nyumbani Ujerumani kupimana ubabe na Celtic kutoka Scotland.

Mabingwa wa Ujerumani Bayer Leverkusen watagaragazana na wageni AC Milan kutoka Italia huku Sporting Braga ya Ureno ikiwa ziarani Uholanzi dhidi PSV Eindhoven.

Share This Article