Usiku wa jana Jumanne Machi 12, 2024, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Daktari Samia Suluhu Hassan aliandaa futari katika uwanja wa Ikulu Jijini Dar es salaam.
Jana ndiyo ilikuwa siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhan na hafla hiyo ilihudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo viongozi, wasanii na makundi mbalimbali ya Kijamii.
Ni katika hafla hiyo hiyo ambapo wanamuziki Diamond Platnumz na Harmonize wanaochukuliwa kuwa mahasimu walisalimiana na kunong’onezana hatua iliyozua msisimuko nchini humo.
Mwanamuziki Rayvanny ambaye aliwahi kusajiliwa na kampuni ya muziki ya Diamond Wasafi alichapisha picha ya taarifa ya salamu za wawili hao na kuweka ishara ya moto.
Harmonize alikuwa pia amesajiliwa kwenye kampuni hiyo ya Wasafi na wakati aliamua kuondoka mambo hayakuwa rahisi kwani alihitajika kulipa hela nyingi.
Masharti ya mkataba wa usajili yalisababisha uhusiano wa wasanii hao wawili kuharibika kabisa hadi walipokutana Ikulu jana.