Dereva wa basi lililosababisha vifo barabara ya Nakuru-Eldoret aachiliwa kwa dhamana

Martin Mwanje & KNA
2 Min Read

Dereva wa basi lililogongana na matatu inayomilikiwa na Northways Sacco kwenye barabara ya Nakuru-Eloret ameachiliwa kwa dhamana. 

Ajali hiyo ilitokea Januari 9, 2024 katika eneo la Twin Bridge katika kaunti ndogo ya Kuresoi Kaskazini na kusababisha vifo vya watu 15.

Watu wengine kadhaa walijeruhiwa na kukimbizwa hospitalini.

Hakimu Mkuu Mwadamizi Daisy Mosse alimwachilia kwa dhamana Clement Kiarie mwenye umri wa miaka 34 baada ya dereva huyo kukanusha mashtaka ya kusababisha vifo vya watu hao.

Hakimu Mosse alisema dereva huyo yuko huru kwenda zake nyumbani akisubiri kusikilizwa kwa kesi hiyo ya jinai baada ya yeye kutoa dhamana ya shilingi milioni moja au dhamana ya kiasi kama hicho cha fedha.

Kiarie anayefanya kazi na kampuni ya mabasi yenye makao yake nchini Uganda kwa jina Classic King anakabiliwa na mashtaka 15 ya kusababisha vifo kwa kuendesha gari kwa njia hatarishi, kukiuka matumizi ya sera ya bima na kubeba abiria 41 wasiokuwa na bima kando na kuendesha gari kizembe.

Alikanusha mashtaka yote dhidi yake.

Awali, upande wa mashtaka ukiongozwa na Patrick Kangethe ulipinga kuachiliwa huru kwa mtuhumiwa ukisema kulikuwa na hatari ya yeye kutoroka ikizingatiwa alifanya kazi na kampuni ya kigeni na itakuwa vigumu kumtafuta.

Kiarie alitoweka baada ya kutokea kwa ajali hiyo na kukamatwa baadaye.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uchukuzi na Usalama Barabarani, NTSA George Njao kupitia taarifa alisema ajali hiyo ilitokana na ukosefu wa nidhamu ya leni na kuendesha gari kwa njia hatarishi kulikofanywa na dereva huyo wa basi wakati akijaribu kuyapita magari mengine.

Martin Mwanje & KNA
+ posts
Share This Article