Idara ya uhalifu wa jinai DCI, imewatambua washukiwa wa genge la majambazi ambao huvunja magari na kuiba bidhaa zilizomo Jijini Nairobi.
Miongoni mwa majambazi hao ni mwanamume wa umri wa miaka 42 Amos Odera Audo, ambaye amenakiliwa na kamera fiche za CCTV katika matukio kadhaa ya uhalifu.
Odera alifumaniwa na kukamatwa katika maficho yake mtaani kaloleni Jijini Nairobi.
Mshirika wake John Musiyo Mbingu, alikamatwa katika majengo ya mahakama ya Kibera alikofika kusikizwa kwa kesi dhidi yake kuhusu kuvunja magari.
Hata hivyo maafisa wa DCI waliomkamata wanasema kuwa mshukiwa huyo alitoroka alipoachiliwa kwa dhmana ya polisi ili atafute matibabu, lakini kibali cha kukamtwa kwake tayari kimetolewa.
Maafisa hao wa polisi wanawasaka washirika wao wawili pamoja na wale ambao hupokea bidhaa hizo za kuibwa.
Kulingana na idarqa ya DCI, majambazi hao wanaaminika kuwa na soko la pamoja la bidhaa za kuibwa, huku wezi hao wakilenga magari ya wateja wa maduka ya jumla, wale wa benki na wanaotoa kiwango kikubwa cha fedha katika benki.
Magari mengine ambayo hulengwa ni yale ambayo yana vitu vya thamani kama vile tarakilishi, simu za bei ghali ambazo huonekana kutoka nje.
Idara ya DCI ilielezea kisa cha wizi wa shilingi milioni 1.5 kutoka kwa mteja wa benki ya DTB, baada ya majambazi kuvunja gari lake aina ya Mazda CX5, katika mtaa wa Parklands Jijini Nairobi.
Katika kisa hicho, mwathiriwa huyo alikuwa ameacha shilingi 466,000 alizokuwa ametoa kwenye benki, tarakilishi ya thamani ya shilingi 105,000 na simu ya mkononi alipotoka kuenda dukani.
Ni kutokana na ongezeko la visa hivyo ndipo idara ya DCI ilipoanza uchunguzi na kusababisha kukamatwa kwa washukiwa hao, huku wakiendelea kuwasaka washukiwa wengine.