DCI yatangaza zawadi ya pesa kwa atakayesaidia kukamatwa kwa Jumaisi

Marion Bosire
1 Min Read

Idara ya upelelezi wa jinai nchini DCI imetangaza zawadi ya pesa kwa yeyote atakayetoa habari muhimu ambazo zitasaidia maafisa kukamata mshukiwa Collins Jumaisi Khalusha.

Kupitia akaunti yake ya mtandao wa X, DCI imetangaza kwamba atakayesaidia katika kumkamata tena mshukiwa huyo mkuu wa mauaji ya Kware huko Embakasi atazawadiwa kiasi ambacho hawakufichua cha pesa.

“Idara ya upelelezi nchini DCI inatafuta usaidizi wa umma katika kupata habari zitakazosaidia kumkamata tena Collins Jumaisi Khalusha.” lilisema tangazo la DCI.

Jumaisi na wenzake 12 walitoroka kutoka korokoro za kituo cha polisi cha Gigiri kaunti ya Nairobi.

Watu hao 12 wanasemekana kuwa raia wa Eritrea ambao walipatikana nchini bila idhini.

Jumanne Agosti 20, 2024 saa 11 asubuhi afisa wa polisi aliyekuwa kwenye zamu katika kituo cha polisi cha Gigiri kwa jina Gerald Mutuku, alizuru seli zote kama ilivyo ada akiwa na msimamizi wa duka la kituo hicho kuwapa washukiwa kiamsha kinywa.

Walipofungua seli walishangaa kupata kwamba hakukuwa na yeyote ndani kwani walihepa baada ya kukata nyaya za eneo ambao huwa wanaotea jua.

Maafisa kadhaa wa polisi wanaofanya kazi katika kituo hicho cha polisi wamesimamishwa kazi kutoa fursa kwa uchunguzi.

Website |  + posts
Share This Article