Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI imekanusha madai ya kuhusika katika kutoweka kwa aliyekuwa Mbunge wa Limuru Peter Mwathi.
Mwathi alisemekana kutoweka punde ya baada ya purukushani kuzuka katika mazishi yaliyohudhiriwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua jana Alhamisi katika eneo la Limuru.
Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, DCI imesema haina nia yoyote ya kumkamata Mwathi inavyodaiwa.
Watu kadhaa walijeruhiwa wakati wahuni waliposhambulia hema alipokuwa ameketi Gachagua wakati Mwathi akitoa hotuba.
Hema na viti ni miongoni mwa vitu vilivyoharibiwa wakati wa purukushani hizo huku waombelezaji akiwemo Gachagua wakilazimika kukimbilia usalama.
Polisi wamesema wameanzisha uchunguzi kubaini kiini na waliohusika na rabsha hizo za jana.