Mkurugenzi wa idara ya upelelezi wa makosa ya jinai (DCI) Mohamed Amin, amethibitisha kujitolea kwa idara hiyo kushirikiana na wadau wengine wa kiusalama katika mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kuhakikisha usalama wa kanda hiyo.
Amin alitoa hakikisho hilo wakati wa mkutano wa nane wa maafisa wakuu wa polisi wa kanda ya Afrika Mashariki, uliong’oa nanga jana Jumatano Jijini Dar es Salaam, nchini Tanzania.
Mkutano huo uliowaleta pamoja wakurugenzi kutoka idara za upelelezi, uhamiaji, magereza na usajili wa magari, ulijadili kwa kina maswala yanayoathiri kanda hiyo, pamoja na utekelezweaji wa maamuzi yaliyopitishwa wakati wa mkutano wa saba wa maafisa hao.
Fauka ya hayo, mkutano huo pia, ulijadili kuhusu ulanguzi wa watu na mihadarati, huku ukifanyia marekebisho ripoti ya silaha ndogondogo kuhusu kutekelezwa kwa makubaliani ya mkutano wa Nairobi katika kanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mkutano huo umeratibiwa kukamilika Oktoba 26,2024.