Idara ya upelelezi wa maswala ya Jinai DCI, imeanzisha uchunguzi katika madai ya ufisadi kwenye mpango wa utoaji wa msaada wa karo katika serikali ya kaunti ya Uasin Gishu.
Hatua hiyo inafuatia malalamishi ya watu wanaodai kutapeliwa mamilioni ya pesa kupitia kwa mpango wa karo za masomo nchini Finland na Canada.
Wazazi na wanafunzi walioathiriwa wametakiwa kuandikisha taarifa katika ofisi ya DCI ya Eldoret tarehe 18 mwezi huu.Wanaombwa kufika ofisini humo na stakabadhi za kuthibitisha malalamishi yao.
Seneta Jackson Mandago aliyekuwa gavana wa kaunti hiyo wakati mpango huo ulipoanzishwa amejitetea huku akimtaka gavana wa sasa asiepuke suala hilo na kuwajibu wazazi.
Kulingana na Mandago, mpango huo ulikabidhiwa serikali ya gavana wa sasa Jonathan Bii ukiwa na zaidi ya shillingi millioni 104 katika akaunti za benki.