Maafisa wa polisi katika kaunti ya Kakamega wanachunguza kisa kimoja ambapo dawa na vifaa muhimu viliibwa katika hospitali ya rufaa ya Kakamega.
Naibu Gavana wa kaunti hiyo Ayub Savula amesema watu wasiojulikana walivunja na kuingia katika ofisi ya afisa msimamizi wa hospitali hiyo na kuvuruga kamera za usalama za CCTV. Alisema waliiba kompyuta iliyokuwa na rekodi muhimu za hospitali hiyo.
Savula amepuuzilia mbali madai kuwa huduma za matibabu zimedumazwa katika hospitali kadhaa kwenye kaunti hiyo kutokana na uhaba wa dawa na bidhaa zingine muhimu.
Ripoti za wizi huo zilichipuka baada ya taarifa kusambaa kwenye mitandao ya kijamii zikidai kuwa idara mbalimbali katika hospitali ya rufaa ya Kakamega zimelazimika kufungwa kutokana na uhaba wa bidhaa muhimu za kufanyia kazi.
Wagonjwa wanaotafuta huduma za matibabu wamelalamika kutokana na hatua ya kutakiwa kununua dawa, glovu na bidhaa zingine muhimu kutoka kwenye famasia za eneo hilo.