Dawa gushi za kuua wadudu waharibifu na magugu zaongezeka nchini

Marion Bosire
1 Min Read

Bodi inayosimamia dawa za kuua magugu nchini PCPB imelalamikia ongezeko la dawa hizo gushi na nyingine ambazo hazijasajiliwa katika soko la humu nchini.

Meneja wa PCPB eneo la Pwani Stanley Ng’ang’a anasema kwamba bodi hiyo imepata habari kuhusu kuingizwa nchini kwa dawa hizo gushi za kuua magugu na wadudu kupitia bandari ya Mombasa.

Nganga aliyekuwa akizungumza huko Mombasa alitaja shehena kadhaa za bidhaa hizo ambazo ziliidhinishwa kuingia nchini kinyume cha sheria wiki jana.

Anasema bodi hiyo ililazimika kuchukua hatua kali ya kutekeleza sheria ya dawa hizo na kudhibiti kuingizwa kwake nchini.

Afisa mkuu wa kuhakikisha sheria hiyo inafuatwa katika PCPB Karisa Mududu anawasihi wakenya kununua dawa za kuua wadudu na magugu kwa wauzaji waliosajiliwa pekee.

Aliongeza kusema kwamba wauzaji wa bidhaa hizo ambao hawatimizi sheria wako katika hatari ya kufungiwa biashara zao.

Kulingana na sheria ya PCPB yeyote anayepatikana akikiuka masharti atahukumiwa kifungo cha miaka miwili gerezani au kutozwa faini ya shilingi 250, 000 au vyote kwa pamoja.

Share This Article