Mwanamuziki wa Nigeria David Adedeji Adeleke maarufu kama Davido ametangaza kwamba atatoa mchango wa Naira Milioni 300 kusaidia watoto yatima kwenye siku yake ya kuzaliwa.
Davido ambaye alizaliwa Novemba 21, 1992, alisema pesa hizo pia zitaelekezwa kwa matumizi ya kurekebisha waathiriwa wa uraibu wa dawa za kulevya nchini Nigeria.
Mwaka 2021 alipokuwa akitimiza umri wa miaka 29, Davido alichangisha fedha kutoka kwa mashabiki na marafiki mchango uliofanikiwa pakubwa ndani ya muda mfupi.
Katika dakika 10 za kwanza, Davido alikuwa amepokea Naira milioni 7 mchango ulioishia Naira milioni 200. Aliongeza milioni 50 zake binafsi kwa pesa hizo na kutoa kama mchango kwa vituo mbali mbali vya watoto yatima.
Mwaka 2022 aliasisi wakfu wa David Adeleke wa kusaidia kuendeleza kazi zake za kusaidia jamii nchini Nigeria.
Davido anatarajiwa kuandaa tamasha la siku yake ya kuzaliwa katika ukumbi wa State Farm mjinii Atlanta, Georgia nchini Marekani.