Daniel Simiu na Agnes Ngetich watamalaki mbio za nyika Bomet

Dismas Otuke
2 Min Read

Mshindi wa nishani ya fedha ya dunia katika mbio za mita 10,000 Daniel Simiu, na mshindi wa nishani ya shaba ya dunia katika mbio za nyika duniani Agnes Jebet Ngetich, wameibuka mabingwa wa kondo wa tatau wa mbio za nyika ulioandaliwa Jumamosi katika uwanja wa Kyongong kaunti ya Bomet.

Jebet alishinda mbio za vidosho alipoziparakasa kwa muda wa dakika 31 sekunde 55 nukta 52,akifuatwa na Cynthia Chepng’eno kwa dakika 32 sekunde 59 nukta 88, huku Sandrafellis Chebet akiridhia nafasi ya tatu kwa dakika 32 sekunde 11 nukta 97.

Simiu alinyakua ubingwa wa mbio za wanaume akitimka kwa dakika 28 sekunde 41 nukta 71, akifuatwa na Edwin Bett kwa dakika 28 sekunde 45 nukta 15, huku Vincent Langat akimaliza wa tatu kwa dakika 28 sekunde 45 nukta 63.

Mercy Chepkoech ameshinda mbio za kilomita 6 wasichana walio chini ya umri wa miaka 20 alipotumia dakika 19 sekunde 24 nukta 88 kukata utepe,akifuatwa na Diana Cherotich kwa dakika 19 sekunde 27 nukta 9 naye Diana Chepkemoi, akaambulia nafasi ya tatu kwa dakika 19 sekunde 57 nukta 67.

Katika mbio za kilomita 8 wavulana wasiozidi umri wa miaka 20,Gideon Kipngetich alinyakua ushindi kwa dakika 23 nukta 85 ,akifuatwa na Mathew Kipkoech kwa muda wa dakika 23 sekunde 7 nukta 54, wakati Kipyegon Korir akichukua nafasi ya tatu kwa dakika 23 sekunde 18 nukta 67.

Mkondo wa nne wa mbio za Nyika nchini utaandaliwa mjini Olkalou Novemba 18 ukifuatwa na ule wa tano na wa mwisho wa Iten wiki moja baadaye.

Website |  + posts
Share This Article