Muungano wa wafanyakazi nchini (COTU) unataka nyongeza ya mishahara ya wafanyakazi kwa asilimia 50 kuwakimu dhidi ya gharama ya juu ya maisha.
Wakizungumza na wanahabari Jumamosi, viongozi hao wa COTU wamesema matozo mapya yamepunguza mishahara ya wafanyakazi na mzigo huo utapunguzwa tu endapo serikali itatoa nyongeza ya asilimia 50.
Naibu katibu mkuu wa COTU Benson Okwaro ametaja nyongeza ya bei ya mafuta iliyotekelezwa wiki hii na kusababisha kuongezwa kwa ada za usafiri kwa magari ya umma kuwa ya ukatili mkubwa kwa Wakenya wote na hususan wafanyakazi.
“Kile tunataka kutoka kwa serikali ni kuongezwa kwa mishahara ya wafanyakazi kwa asilimia 50 ndiposa wajikimu dhidi ya ushuru unaotozwa kwa sasa kutoka kwa mishahara na kuwawezesha kumudu gharama ya juu ya maisha. Ikiwa serikali haitatusikiza, basi tuko tayari kuitisha mgomo wa wafanyakazi wote nchini,” akasema Okwaro.
COTU pia imeitaka serikali kuvunjilia mbali tume ya kuratibu mishahara ya wafanyakazi, SRC wakidai inalenga kuangamiza vyama vya wafanyakazi kinyume cha sehria za Kenya na muungano wa wafanyakazi ulimwenguni.
Katibu mkuu wafanyakazi katika sekta ya kawi (KETAWU) Ernest Nadome amemtaka Rais William Ruto kutafakari upya na kuimarisha maslahi ya wafanyakazi.
“Mfanyakazi wa Kenya amekandamizwa kupita kiasi na hali imekuwa ngumu zaidi na hatua ya SRC kukandamiza vyama vya wafanyakazi ambayo havipewi fursa ya kujadiliana na waajiri kuhusu nyongeza ya mishahara.”