Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi nchini (COTU) unataka mazungumzo ya kurekebisha makato ya bima mpya ya afya ya jamii, SHIF na yale ya ujenzi kutoka kwa mishahara ya wafanyakazi.
Akizungumza katika kaunti ya Nairobi, Naibu Katibu Mkuu wa COTU Benson Okwaro amesema ipo haja ya kufanya marekebisho ya makato hayo mawili kutoka kwa mshahara wa kimsingi, badala ya sasa ambapo makato hayo yanatolewa kwenye mshahara wa jumla.
Okwaro amesema mazungumzo kati ya serikali, vyama vya wafanyakazi na waajiri ili kurekebisha mfumo huo mpya wa makato ndio njia pekee ya kuwapunguzia wafanyakazi mzigo wa ushuru.
Hii ni baada ya Tume ya Mishahara na Marupurupu nchini, SRC kuzuia nyongeza ya mishahara kwa wafanyakazi.
Makato mapya ya SHIF yameanza kutekelezwa mwezi huu, ambapo kila mfanyakazi anachangia asilimia 2.75 kutoka kwa mshahara wa jumla.
Wafanyakazi wengi wamelalamikia hatua hiyo ambayo imepunguza malipo yao kwa kiwango kikubwa.