Mwanamuziki wa Uganda Cindy Sanyu ameshauri wasanii chipukizi waangazie kazi zao ili kuhakikisha ni bora kwa ajili ya mashabiki zao.
Akizungumza kwenye mahojiano, rais huyo wa chama cha wanamuziki wa Uganda UMA alitoa ushauri huo kama jibu kwa lalama za wasanii chupukizi kwamba wasanii waliobobea huwa vizingiti kwa mafanikio yao.
Kulingana na Cindy, tasnia ya muziki haina maeneo maalum kwa kila mmoja bali ni fursa ziko huko kwa watakaotia bidii na kutolea mashabiki zao kazi safi.
“Usiangazie watu wengine ukidhani kwamba wanakuwa vizingiti. Mashabiki wanataka tu burudani. Wape burudani na utapata kazi nyingi.” Alishauri Cindy.
Usemi wa Cindy unajiri wakati ambapo kuna mvutano unaoendelea mitandaoni kati ya Ava Peace na Sheebah Karungi, ambapo Ava anamlaumu Sheebah kwa kumhujumu katika tumbuizo fulani.
Cindy anaamini kwamba msanii anapokuwa na muziki ambao ameandaa vyema, hakuna mtu anaweza kumzuia kuafikia ufanisi akiongeza kusema kwamba wanafaa kutupilia mbali mawazo kwamba wanahujumiwa.
“Ukweli ni kwamba ukiwapa watu wanachokitaka, watakuita na kukupa kazi. Hilo ndilo la maana. Kila kitu kingine ni kelele tu” aliendelea kusema Cindy.
Kingine alichokisema ni kwamba wasanii chipukizi wanafaa kuchukulia kama sifa, majina yao yanapotajwa pamoja na majina ya wasanii waliobobea, iwe ni kwa uzuri au kwa ubaya.
