Rais William Ruto ametoa changamoto kwa Chuo Kikuu cha kitaifa cha mafunzo ya ulinzi (NDU-K), kuendeleza maono yake ya kubuni mikakati ya kukabiliana na changamoto ibuka na kudhibiti majanga hasa wakati taifa linapokumbwa na mizozo.
Akizungumza leo Ijumaa wakati wa sherehe ya kufuzu katika Chuo Kikuu hicho mjini Lanet, kaunti ya Nakuru, kiongozi wa taifa alikitaka chuo hicho kuandaa mifumo ya usimamizi bora wa majanga nchini.
“Natoa changamoto kwa chuo kikuu cha mafunzo ya ulinzi kushikilia maono yake ya kubuni mikakati ya kukabiliana na changamoto ibuka,” alisema Rais Ruto.
Aidha Rais Ruto alihimiza chuo hicho kuzingatia ushirikiano na serikali za kaunti, kama njia ya kuimarisha utayari na ufanisi wa mifumo ya kukabiliana na majanga hapa nchini, yakiwemo majanga yanayohusiana na mabadiliko ya hali ya hewa.
“Ninahimiza Chuo Kikuu hiki kushirikiana na serikali za kaunti ili kukabiliana kikamilifu na majanga hapa nchini hasaa yale ya Mabadiliko ya Tabia Nchi,” aliongeza Rais Ruto.
Rais aliwapongeza wanafunzi waliofuzu kwa kujitolea kwao kulinda usalama wa nchi hii.
Alisema usalama wa taifa hili unategemea ushirikiano wa nchi hii na majirani wa kanda hii pamoja na washirika wengine duniani.