Mwigizaji mkongwe wa filamu za Nollywood nchini Nigeria Chiwetalu Agu, ametoa ushauri kwa vijana ambao wana tabia ya kuumiza wapenzi wao, kuwaacha na kuendelea na maisha kana kwamba hakuna kilichofanyika.
Agu ambaye hupenda kuonyesha kwenye mitandao ya kijamii jinsi anampenda mke wake, alichapisha video ambapo anasimulia kisa cha msichana fulani.
Mkongwe huyo anasimulia jinsi binti huyo alimtoa uhai aliyekuwa mpenzi wake baada ya kumuacha ghafla.
Kulingana na mzee huyo sio kila mmoja ana moyo wa kusamehe na kuachilia waliomkosea, akiongeza kwamba wafu hawawezi kusimulia kilichotokea.
“Ombeeni vijana, na mwashauri wasicheze na hisia za wengine.” alisema mzee huyo.
Alifafanua kwamba haungi mkono alichokifanya msichana huyo lakini anaelewa kwamba aliumizwa na akashindwa kumsamehe mpenzi wake wa zamani.
Agu ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 68 amekuwa akiigiza kwa miaka zaidi ya 31 na alianzia kwenye vipindi vya runinga nchini Nigeria kabla ya kuingilia filamu.
Ameigiza kwenye filamu nyingi tu kuanzia kwa “Last Ofalla” ya mwaka 2002 hadi Agbommma ya mwaka 2016.
Oktoba 2021, mzee huyo alijipata pabaya kisheria baada ya kukamatwa na maafisa wa polisi baada ya kuvaa mavazi ya kuunga mkono watu wa jimbo la Biafra.
Kundi la wakazi wa jimbo la Biafra limepigwa marufuku nchini Nigeria kwa sababu ya shinikizo zao za kutaka kujitenga na taifa la Nigeria na kuunda taifa la Biafra.