China yaipa Kenya ruzuku ya shilingi milioni 259 kukabiliana na Ebola na kiangazi

Balozi Guo alisema hatua hiyo ni kutokana na ushirikiano wa karibu na wa kindugu kati ya serikali ya China na serikali ya Kenya na raia  wake.

Dismas Otuke
1 Min Read

Serikali ya China imeipa Kenya ruzuku ya shilingi milioni 259 kukabiliana na ugonjwa wa Ebola na kiangazi, siku moja baada ya kisa cha kwanza cha Ebola kuripotiwa nchini.

Kati ya ruzuku hiyo, shilingi milioni 129.5 zitaelekezwa kwa kukabiliana na Ebola huku kiwango kingine sawia kikitumika kukabiliana na kiangazi.

Pesa hizo ambazo ni dola milioni mbili za Kimarekani, zilikabidhiwa Katibu wa Wizara ya Fedha Dkt. Chris Kiptoo siku ya Alhamisi na Balozi wa China  nchini Kenya, Guo Haiyan.

Hafla hiyo ilishuhudiwa pia na Katibu wa Afya ya Umma Mary Muthoni.

Pesa hizo zitaimarisha juhudi za kukabiliana na Ebola katika kaunti zinazoorodheshwa kuwa na hatari kubwa ya maambukizi na pia kupiga jeki juhudi za kutoa misaada ya kibinadamu katika maeneo kame nchini Kenya.

Balozi Guo alisema hatua hiyo ni kutokana na ushirikiano wa karibu na wa kindugu kati ya serikali ya China na serikali ya Kenya na raia  wake.

Share This Article