China imeipatia Kenya msaada wa shilingi bilioni 1.8 (RMB milioni 100) zitakazotumiwa katika kuboresha hospitali mbalimbali za umma humu nchini.
Makubaliano ya utoaji wa msaada huo yalitiwa saini leo Alhamisi kati ya Waziri wa Fedha John Mbadi na Balozi wa China humu nchini Guo Haiyan katika makao makuu ya Wizara ya Fedha jijini Nairobi.
Wizara ya Fedha imetaja msaada huo kuwa muhimu mno katika juhudi za serikali ya Kenya Kwanza kuboresha utoaji huduma katika hospitali za umma.
Hususan, fedha hizo zitatumiwa kuboresha hospitali mbalimbali ikiwa ni pamoja na hospitali ya rufaa ya Londiani na ile ya rufaa ya Baringo.
Hospitali zingine zitakazonufaika ni zile za Kilifi, Misikhu na Bildad Kagia, na Chuo cha Mafunzo ya Wakulima cha Kaimosi.
Wakati wa hafla hiyo, Waziri Mbadi aliishukuru serikali ya China kwa msaada wake endelevu kwa Kenya, akisisitiza kuwa ushirikiano huo unaashiria uhusiano thabiti uliopo kati ya Kenya na China.
Msaada huo unakuja wakati ambapo Kenya imeimarisha juhudi za kuhakikisha raia wake wote wanapata huduma bora za afya.
Kenya inalenga kufikia lengo hilo kupitia bima ya matibabu inayotolewa kupitia Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) iliyozinduliwa nchini humo mwaka jana.