Rais wa China Xi Jinping amesema kwamba taifa lake liko tayari kushirikiana na Marekani.
Alikuwa akizungumza alipokutana na Rais anayeondoka wa Marekani Joe Biden katika kongamano la ushirikiano kati ya Asia na Pacific.
Alisisitiza umuhimu wa heshima kudumu kati ya mataifa hayo mawili akionekana kurejelea utawala ujao wa Marekani wa Donald Trump.
Xi hakutaja jina la Trump kwenye mazungumzo hayo na alimpigia simu Novemba 6, 2024 kumpongeza baada ya ushindi katika uchaguzi wa Urais wa Marekani.
kulingana naye lengo la China la kuwa na uhusiano thabiti, mzuri na endelevu na Marekani halijabadilika huku akionya kwamba iwapo nchi hizo zitashikilia ushindani na kuumizana basi uhusiano wao utaharibika.
Katika kipindi cha kwanza cha Trump uongozini kati ya mwaka 2017 na 2021, kulikuwa na mvutano kati ya China na Marekani ambapo ushuru uliongezwa kwa bidhaa za China zilizoingizwa Marekani.
China nayo iliweka ushuru na vikwazo vingine vya kibiashara dhidi ya Marekani, hatua zilizochukuliwa na wataalamu kuwa pigo kwa chumi hizo mbili.
Wakati wa kampeni, Trump aliahidi kulinda watengenezaji bidhaa wa Marekani dhidi ya ushindani wa China.
Alidhihirisha pia ujasiri kwamba Marekani itapatana na China hata baada ya kuitoza ushuru wa juu alipokuwa madarakani.
Kulingana na Trump Xi alikuwa mungwana hadi janga la Covid 19 lilipojiri kwani alimlaumu kwa kukubalia ugonjwa huo kusambaa.
Xi amekuwa akiongoza China tangu mwaka 2013 na chini ya uongozi wake, sheria ya kuwa madarakani kwa mihula miwili pekee iliondolewa, jambo linalomvutia Trump.