Leo tutakamilisha msururu wa kuangazia historia ya michezo ya Olimpiki kwa sehemu ya tatu, na ya mwisho ikijumuisha makala ya mwaka 2004 hadi 2020.
Makala ya mwaka huu ambayo ni ya 33 yanaandaliwa nchini Ufaransa na yatafunguliwa rasmi kesho nchini Ufaransa.
Mji wa Athens Ugiriki uliandaa mashindano ya Olimpiki ya mwaka 2004 ambapo mataifa 201 yalishiriki.
Mwogeleaji wa Marekani Michael Phelps aliweka historia kunyakua medali nane zikiwemo dhahabu sita katika michezo hiyo.
Kenya ilishinda dhahabu 1 fedha 4 na shaba 2 katika mashindano hayo Ezekiel Kemboi, akishinda dhahabu yake ya kwanza katika mita 3,000 kuruka viunzi na maji.
Michezo ya mwaka 2008 iliandaliwa barani Asia katika mji wa Beijing ,China.
Historia iliandikishwa upya katika michezo hiyo rekodi 40 za dunia zikivunjwa, na nyingine zaidi ya rekodi 130 za Olimpiki zikiandikishwa upya.
Kenya ilisajili matokeo bora katika historia ya Olimpiki kwa dhahabu 6 fedha 4 na shaba 6 .
Marehemu Samuel Wanjiru alinyakua dhahabu ya kwanza ya Kenya ya mbio za marathon, huku pia Pamela Jelimo na Nancy Lagat wakishinda dhahabu za kwanza kwa Kenya katika mita 800 na mita 1500 wanawake mtawalia.
London Uingereza ilikuwa mwenyeji wa mashindano ya mwaka 2012, ndondi ya wanawake ikijumuishwa kwa mara ya kwanza huku baseball na Softball zikienguliwa .
Kenya iliajili dhahabu 1 fedha 4 na shaba 7 .
Baadaye mwaka 2016 michezo ililekezwa mjini Rio De Janeiro Brazil ikiwa mara ya kwanza kuandaliwa barani Amerika Kusini.
Raga ya wanawake iliandaliwa kwa mara ya kwanza huku gofu ikirejeswa baada ya kukosekana kwa miaka 112, nayo raga ya wanume ikirejea baada ya miaka 92.
Kenya iisajili matokeo mazuri kwa dhahabu 6 fedha 4 na shaba 1.
Makala ya mwisho ya mwaka 2020 yalistahili kuandaliwa Tokyo, lakini yakaahirishwa hadi mwaka 2021 kutokana na chamko la virusi vya Corona.
Mashabiki kwa mara ya kwanza hawakuruhusiwa uwanjani huku wachezaji na maafisa wakilazishwa kuvalia barakoa kama njia ya kuzuia maambukizi .
Kenya ilinyakua dhahabu 4 ,fedha 4 na shaba 2,Faitha Kipyegon akiwa mwanamke wa kwanza kuhifadhi taji ya mta 1500, wakati Peres Jepchirchir akiwa mwanamke wa kwanza wa Kenya kunyakua dhahabu ya marathon.
Hadi sasa Kenya ndio nchi iliyo na ufanisi mkubwa katika michezo ya Olimpiki barani Afrika kwa dhahabu 35, fedha 42 na shaba 36.