Makala ya 33 ya michezo ya Olimpiki inayoandaliwa kila baada ya miaka minne, yataanza rasmi leo Julai 24 jijini Paris,Ufaransa kwa mechi za mchezo wa Raga ya wanaume saba upande na pia soka ya wanaume.
Katika sehemu ya pili ya makala ya Chimbuko la Olimpiki leo tutaangazia makala ya mwaka 1976 hadi mwaka 2000 .
Michezo ya Olimpiki ya mwaka 1976 iliandaliwa mjini Montreal,nchini Canada ikiwa mara ya kwanza kuandaliwa nchini humo na fani za mpira wa kikapu kwa wanawake,mpira wa pete na upigaji makasia zilijumuishwa kwa mara ya kwanza.
Michezo hiyo itasalia kwenye daftari za historia baada, ya kususiwa na takriban mataifa 20 ya Afrika yakipinga ubaguzi wa rangi.
Nchi hizo zilizosusia mashindano ziliongozwa na Tanzania,kupinga hatua ya kamati ya kimataifa ya Olimpiki IOC kuruhusu timu ya raga ya New Zealand kushiriki, licha ya kuunga mkono ubaguzi wa rangi uliokuwa ukitekelezwa nchini Afrika Kusini.
Kenya pia haikushiriki makala hayo.
Mwaka 1980 michezo iliandaliwa mjini Moscow Urusi ambapo Kenya ilijiunga na mataifa 70 kususia mashindano .
Mgomo huo uliongozwa na Rais wa Marekani wakati huo Jimmy Carter, wakipinga uvamizi wa Muungano wa Usovieti dhidi ya Afghanistan.
Mashindano hayo yalikuwa na nchi 80 pekee zilizoshiriki ikiwa idadi ndogo zaidi kuwahi kushiriki.
Los Angeles walikuwa wenyeji wa mashindano ya mwaka 1984 huku Muungano wa Usovieti, pia uliongoza mgomo wa mataifa ya Mashariki mwa Ulaya kushiriki kulipiza kisasi dhidi ya Marekani waliosusia mashindano iliyoandaa.
Kenya ilishiriki na kuzoa medali tatu,dhahabu moja na shaba 2.
Hali ya msukosuko iliendelea katika michezo ya mwaka 1988 iliyoandaliwa mjini Seoul Korea Kusini,Korea Kaskazini ikiteta kunyimwa kuwa mwandalizi mwenza.
Ni katika makala hayo ambapo mchezo wa Table Tennis ulijumuishwa kwa mara ya kwanza.
Kenya ilizoa dhahabu tano kwa mara ya kwanza ,fedha mbili na shaba mbili ,ikiwemo dhahabu ya pekee hadi leo katika ndondi iliyotwaliwa na marehemu Robert Wangila.
Pia ni hapo ambapo Douglas Wakihuri alishinda nishani ya fedha ikiwa ya kwanza katika mbio za marathon.
Mji wa Bercelona Uhispania uliandaa mashindano ya mwaka 1992, Baseball ukijumuishwa kwa mara ya kwanza sawia na Badminton na Judo ya wanawake
Kenya ilinyakua dhahabu 2 fedha 6 na shaba 2 katika michezo hiyo ambayo ilishuhudia pia Muungano wa Usovieti ukivunjwa na kuzaa mataifa 16.
Marekani ilitwikwa jukumu la kuandaa makala ya mwaka 1996 lakini safari hii katika mji wa Atlanta.
Michezo hiyo ilikumbwa na shambulizi la kigaidi lililowauwa watu wawili huku wengine 110 wakijeruhiwa.
Hata hivyo mhusika mkuu wa shambulizi hilo Eric Rudolph,alikamatwa mwaka 2003,takriban miaka 17 baadaye.
Fani za voliboli ya ufukweni soka ya wanawake ,uendeshaji baiskeli na Softball zilijumuishwa kwa mara ya kwanza.
Kenya ilinyakua dhahabu moja fedha 4 na shaba 3 katika makala hayo.
Sydney Australia ilikuwa mwandalizi aliyefuatia wa michezo ya mwaka 2000, Marion Jones wa Marekani akiwashangaza wengi aliponykua dhahabu 5 katika mbio za masafa mafupi.
Ni hapa ambapo Taekwondo na triathlon zilijumuishwa huku wanawake wakishiriki kwa mara ya kwanza katika michezo ya weightlifting na modern pentathlon .
Kenya ilinyakua dhahabu 2 fedha 3 na shaba mbili ,Joyce Chepchumba akiwa mwanamke wa kwanza kutoka humu nchini kunyakua medali ya shaba ya mbio za Marathon.