Cheruiyot,Komen na Kipkorir wafuzu kwa nusu fainali 1,500 Olimpiki

Dismas Otuke
1 Min Read

Wakenya wote watatu Timothy Cheruiyot, Brian Komen na  Reynold Cheruiyot Kipkorir, wamefuzu kwa nusu fainali ya mbio za 1,500m,  katika siku ya kwanza ya riadha ya uwanjani michezo ya Olimpiki Jijini Paris Ufaransa.

Komen ambaye ni bingwa wa Afrika alistahimili ukinzani mkali, kabla ya kumaliza wa pili katika mchujo wa kwanza siku ya Ijumaa uwanjani Stade de France’s, akitumia  dakika 3 sekunde  36.31, nyuma ya Mwingereza  Josh Kerr, aliyeibuka mshindi kwa dakika  3 sekunde 35.83.

Cheruiyot, ambaye ni bingwa wa Dunia mwaka  2019 na pia mshindi wa nishani ya fedha ya Olimpiki jijini Tokyo, alikuwa na kibarua kigumu, kabla ya kumaliza katika nafasi ya tano kutoka mchujo wa pili akitumia dakika 3 sekunde 35 .39.

Reynold Kipkorir Cheruiyot alimaliza wa nne katika mchujo wa tatu na wa mwisho  kwa dakika 3 sekunde 37.12 ,nyuma ya bingwa mtetezi Jakob Ingebrigsten kutoka Norway aliyemaliza wa tatu.

Wanariadha waliomaliza nje ya nafasi sita za mwanzo kinyume na awali wamepewa nafasi ya kushirki mchujo mwingine kesho, ili kuwania tiketi ya kufuzu kwa semi fainali ya Jumapili.

Share This Article