Mpanda milima kutoka Kenya Cheruiyot Kirui , ambaye alikuwa ameripotiwa kupotea katika ziara zake za kupanda Mlima Everest siku ya Jumatano, amepatikana huku ameaga dunia mita chache chini ya kilele cha Mlima Huo.
Mwili wake uligunduliwa katika eneo hatari linalojulikana kama eneo la kifo kama ilivyoripotiwa na maafisa wa eneo hilo huko Nepal.
Kulingana na maafisa wa Kampuni ya wapanda milima inayofahamika kama Seven Summit Treks (SST), Kirui alitoka nje ya kambi ya Bishop Rock iliyoko kwenye mwinuko wa mita 8,000 siku ya Jumatano kabla ya kupoteza mawasiliano nao.
“Nawang ambaye alikuwa pamoja na Kirui alikuwa amewasiliana mara ya mwisho na maafisa wa kambi yetu akisema kwamba Kirui alikuwa amekataa kushuka Mlima huo na hata kuamua hatatumia oksijeni ya ziada. Nawang pia alisema Kirui alikuwa akionyesha tabia zisizo za kawaida,” maafisa wa SST walisema katika ripoti yao.
Ripoti hiyo pia iliongeza kuwa katika mahojiano mwezi uliopita, Kirui alidokeza kuhusu lengo lake la kujaribu kupanda Mlima Everest, ambao ni mlima mrefu zaidi duniani bila oksijeni ya ziada.
“Changamoto kwangu itakuwa kupanda Mlima Everest bila oksijeni ya ziada. Hata hivyo, sitahisi kama nimepata mafanikio yoyote bila kufanya hivyo. Nataka kuona jinsi mwili wangu utaweza kukabiliana na mwinuko kama huo.” Kirui alisema kwenye mahojiano hayo.
Cheruiyot Kirui alikuwa mpanda milima mwenye uzoefu Kwa Kuwa hapo awali, alikuwa amefanikiwa kupanda milima kama vile Mlima Kenya Na Mlima Kilimanjaro ambao ni Mlima mrefu zaidi barani Afrika.