Seneta wa kaunti ya Nandi Samson Cherarkey amechukua hatua ya kutetea Wakenya walioathiriwa na mafuriko pamoja na wale waliokwama katika eneo la Mashariki ya Kati.
Cherarkey amefanya hivyo kwa kuwasilisha ombi la taarifa kutoka kwa kamati ya bunge kuhusu usalama wa taifa, ulinzi na mahusiano ya kimataifa kuhusiana na masuala hayo.
Kiongozi huyo anasema kwamba mvua hutarajiwa kila mara lakini uharibifu uliosababishwa na mvua hivi maajuzi ni dhihirisho la kushindwa kwa utawala kusimamia mfumo wa kupitisha maji taka na kujiandaa kwa majanga.
Anaitaka kamati hiyo iwasilishe ripoti bungeni kuhusu idadi ya vifo, majeruhi na thamani ya mali iliyoharibiwa na mafuriko kuanzia usiku wa Machi 6, 2026.
Kamati hiyo inatakiwa pia kufahamisha Maseneta kuhusu hali ya sasa ya hazina ya kitaifa ya fidia ya majanga na mipango ya fidia kwa waathiriwa.
Kuhusu Wakenya walio ughaibuni, Cherarkey ameangazia gharama kubwa ya kusafirisha miili ya wanaofia huko huku familia zao zikishindwa kabisa kuimudu.
Anasema familia nyingi huchelewesha mazishi, kuchangisha pesa hadharani au hata kuacha kabisa mipango ya kurejesha miili ya wapendwa wao nchini kutokana na gharama ya juu.
Seneta huyo wa Nandi anaitaka serikali kuanzisha hazina ya kusaidia Wakenya kusafirisha miili ya wapendwa wao hadi humu nchini kwa ajili ya mazishi.
Amependekeza pia kwamba Wizara ya Mambo ya Nje ishirikiane na Wizara ya Leba kuhakikisha wahamiaji wa asili ya Kenya wanalindwa na bima au waajiri kusimamia gharama ya kuwarejesha nchini.