Mshikilizi wa rekodi ya Dunia Beatrice Chepkoech, bingwa wa Dunia Mary Moraa na Aaron Cheminingwa walitwaa dhahabu katika michezo ya Afrika inayoendelea nchini Ghana Jumatano usiku.
Chepkoech alinyakua dhahabu ya mita 3000 kuruka viunzi na maji aliweka rekodi mpya ya mashindano ya dakika 9 sekunde 15 .61, akilipiza kisasi baada ya kukosa nishani katika fainali ya mita 5,000 mapema wiki hii.
Peruth Jemutai wa Uganda alinyakua fedha huku Lomi Muleta wa Ethiopia akiridhia shaba.
Moraa,ambaye anatumia mashindano hayo kujiandaa kwa michezo ya Olimpiki alishinda dhahabu ya mita 400 kwa sekunde 50.57, huku fedha ikimwendea Esther Elo wa Nigeria Sita Sibiri wa Burkina Faso akinyakua shaba .
Aaron Cheminingwa alikuwa mwanaume wa kwanza kushinda dhahabu katika makala ya mwaka huu katika mita 800 kwa dakika 1 sekunde 45.72 ,akifuatwa na Alex Kipngetich aliyeshinda fedha wakati Nkape Tumo wa Botswana akinyakua shaba.
Kenya ni ya 11 katika msimamo wa nishani kwa medali 20 dhahabu 4 ,fedha 5 na shaba 11 nyuma ya watani wa jadi Ethiopia walio na dhahabu 5 fedha 4 na shaba 3.
Misri ingali kuongoza kwa medalia 176 dhahabu 92 fedha 41 na shaba 34.
Nigeria ni ya pili kwa medali 90 dhahabu 35,fedha 23 na shaba 38, huku Afrika Kusini ikikalia nafasi ya tatu kwa dhahabu 29 fedha 30 na shaba 38 .
Mashindano hayo yatakamilika Ijumaa hii.