Mshindi wa dhahabu mbili za Olimpiki, Beatrice Chebet, amesema analenga kushinda dhahabu mbili za mita 5,000 na mita 10,000 katika mashindano ya Riadha Ulimwenguni mwaka huu jijini Tokyo, Japani.
Chebet amesema baada ya kushinda dhahabu za Olimpiki na dhahabu za mashindano ya dunia ya mbio za nyika, kilichosalia ni dhahabu ya dunia.
“Tayari nimeanza mazoezi na baada ya kufunga mwaka kwa rekodi ya dunia, ninajiandaa kuanza msimu kwa mashindano ya Xiamen Diamond League, kabla ya kushiriki trials,” amesema Chebet.
Hata hivyo ameongeza kuwa hana lengo la kuvunja rekodi yoyote ya dunia mwaka huu.
“Rekodi za dunia zipo kwa ajili ya kuvunjwa, lakini mwaka huu lengo langu kubwa ni kunyakua dhahabu ya dunia ikiwa tu ndio medali ninakosa hadi sasa.”
Hii inaashiria kuwa majaribio ya kitaifa ya mita 5,000 na 10,000 yatakuwa na ushindani mkubwa kati ya Chebet, Anges Jebet Ng’etich na bingwa mtetezi wa dunia katika mita 5,000, Faith Kipyegon.
Makala ya 20 ya mashindano ya riadha duniani yataandaliwa jijini Tokyo, Japani, mwezi Septemba.