Wizara ya Afya itatoa kwa awamu tatu, chanjo ya dharura ya Polio kwa lengo la Kufikia watoto milioni 7.4.
Awamu ya kwanza ya kampeni hiyo dhidi ya ugonjwa wa kupooza inayolenga watoto wa umri wa chini ya miaka mitano, itazinduliwa Alhamisi, Agosti 24 hadi 28, 2023 kwenye kaunti za Kiambu, Nairobi, Kajiado na Garissa ambapo lengo ni kutoa chanjo kwa watoto milioni 1.8.
Akizungumza kwenye kikao cha wanahabari na wadau, katibu wa afya ya umma Mary Muriuki, alisema Wizara ya Afya imetambua kaunti 10 zilizo kwenye hatari kubwa ya maambukizi ya polio.
Kaunti hizo ni Nairobi, Kiambu, Kajiado, Garissa, Kitui, Machakos, Tana River, Lamu, Wajir na Mandera zitakazohusishwa kwenye mpango wa dharura wa utoaji chanjo.
Alisema awamu ya pili na ya tatu zitakazoandaliwa kati ya mwezi Septemba na Oktoba mwaka huu, zinalenga watoto milioni 2.8 katika kila mojawapo ya kaunti za Kiambu, Nairobi, Kajiado, Garissa, Lamu, Tana River, Wajir, Mandera, Kitui na Machakos.
Hatua ya kuanzisha mpango wa dharura wa kutoa chanjo dhidi ya Polio ilichochewa na ugunduzi wa visa 6 vya ugonjwa huo kwa watoto kwenye kambi ya wakimbizi ya Hagadera, kaunti ya Garissa.