Shule ya msingi ya wasichana ya St. Anne’s Mumias inakabiliwa na changamoto kubwa ya miundombinu.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Sirila Sanya anasema hii inafanya iwe vigumu kutekeleza mfumo mpya wa elimu wa CBC unaojumuisha shule ya sekondari ya chini, JSS.
Sanya sasa anaitaka serikali kuongeza mgao wa fedha unaotolewa kwa shule katika jitihada za kukidhi matakwa ya mfumo huo.
Kando na madarasa, anasema shule hiyo pia inakabiliwa na uhaba wa walimu ambapo walipata walimu 4 pekee wa JSS kuhudumia wanafunzi 258.
Ripoti zinaonyesha kuwa shule nyingi za umma zinakabiliwa na changamoto za uhaba wa madarasa, maabara, walimu na vifaa vya kujifunzia.
Jopo la Elimu la Kuangazia Mageuzi katika Sekta ya Elimu Nchini, PWPER tayari limemkabidhi Rais William Ruto ripoti yake yenye kurasa 392.
Ripoti hiyo inatoa mapendekezo mbalimbali yanayopaswa kutekelezwa ili kufanikisha utekelezaji wa mfumo wa CBC ambao wengi wanasema ni ghali.
Miongoni mwa mapendekezo hayo ni uongezaji wa ufadhili unaotolewa kwa shule za umma ili kufanikisha utekelezaji wa mfumo huo.
Kwenye mapendekezo yake, jopo hilo lenye wanachama 53 chini ya uongozi wa Prof. Raphael Munavu liliitaka Taasisi ya Uendelezaji wa Mitaala Nchini, KICD kupunguza idadi ya masomo yanayotolewa chini ya CBC.
Wizara ya Elimu nayo imetakiwa kuanzisha matumizi ya mfumo wa Kina wa Shule unaoanzia PP1 hadi Gredi ya 9. Mfumo huo unajumuisha shule ya chekechea, shule ya msingi na shule ya chini, zote zitakazosimamiwa kama taasisi moja.
Imependekezwa matumizi ya neno “sekondari” yafutiliwe mbali kutoka shule ya sekondari ya chini ya sasa na ile ya sekondari ya juu.
Kadhalika, jopo liliitaka KICD kupunguza idadi ya masomo kutoka 9 hadi 7 katika shule ya msingi ya chini, 12 hadi 8 katika shule ya msingi ya juu na 14 hadi 9 katika shule ya chini ili kuwapunguzia walimu na wanafunzi mzigo. Masomo katika shule ya chekechea yamependekezwa kuwa 5 ilhali katika sekondari ya juu kuwa 7.
Jopo pia liliitaka Wizara ya Elimu kufutilia mbali uainishaji wa sasa wa shule za umma kama za kitaifa, shule maalum za kaunti, shule za kaunti na kaunti ndogo na badala yake kutumia uainishaji unaozingatia taaluma wanazopendelea wanafunzi katika shule za sekondari ya juu.
Rais Ruto ameitaka Wizara ya Elimu kufanya kila iwezalo kuhakikisha ripoti hiyo inatekelezwa kikamilifu.