Video ambayo imekuwa ikisambazwa mitandaoni inamwonyesha mwanamuziki wa Uganda Jose Chameleone akiimba jukwaani katika tamasha ya Afrofest nchini Canada.
Lakini anaonekana akiwa ameketi kwenye kiti huku akiimba labda kwa sababu bado hajarejesha nguvu mwilini. Mwanamuziki huyo ambaye jina lake halisi ni Joseph Mayanja, amelazwa hospitalini kwa muda nchini Marekani.
Alipoingia jukwaani, Chameleone alijitambulisha kwa njia ya kipekee ambapo anasikika akisema, “Nimekuja na muziki kutoka kwa watu wangu, nimekuja na ujumbe kutoka kwa watu wangu kwa sababu ni Afrofest. Nimekuja na uafrika mwingi. Nataka kuwapeleka Afrika. Jina langu ni Jose Chameleone”.
Mwanamuziki mwenza Gravity Omutujju alijitokeza maajuzi na kusihi wapenzi wa muziki nchini Uganda wamwombee Chameleone kwa sababu alikuwa akiugua.
Babake mzazi naye alithibitisha hilo na kuongeza kwamba walikuwa wanapitia wakati mgumu kama familia.