Mwanamuziki wa Uganda Jose Chameleone amependekeza maridhiano kupitia upatanisho kati ya wanamuziki wenza Alien Skin na kakake Pallaso.
Chameleone ambaye anaendelea kupokea matibabu nchini Marekani alirejelea wawili hao wanaozozana kama kaka zake huku akitaka wapatanishwe ili kumaliza tofauti zao.
Alimshukuru naibu mwenyekiti wa chama tawala nchini Uganda NRM wa eneo la mashariki mwa taifa hilo Mike Mukula, kwa juhudi zake za kupatanisha wawili hao.
Jingine alilopendekeza Chameleone ni kuandaliwa kwatamasha la pamoja la wawili hao.
Tayari Mukula ambaye pia aliwahi kuwa waziri wa afya nchini Uganda anaripotiwa kuandaa mkutano wa kupatanisha wawili hao na anaripoti kwamba wako tayari kuzika tofauti zao.
Haya yanajiri siku chache tu baada ya Pallaso na marafiki zake kuvamia makazi ya Alien Skin ambapo walisababisha hasara na kuacha mtu mmoja na majeraha.
Pallaso kaka mdogo wa Jose Chameleone anasemekana kufanya hivyo kama njia ya kulipiza kisasi baada yake kuzozana na Alien Skin kwenye tamasha fulani.
Alien alipiga ripoti polisi ambao walitoa taarifa kwamba wanamsaka pamoja na wenzake.
Kisa hicho pia kilisababisha maafisa wa polisi kupunguza idadi ya watu au walinzi ambao mwanamuziki anakubaliwa kuandamana nao kwa wakati mmoja.
Msemaji wa polisi wa eneo la Kampala Metropolitan Patrick Onyango alitangaza kwamba kila mwanamuziki anaruhusiwa tu kuwa na watu watano.