Chama cha kisiasa cha wiper kimemtimua Farah Maalim, mbunge wa eneo la Dadaab.
Haya ni kulingana na kiongozi wa chama hicho cha Wiper Kalonzo Musyoka, aliyesema hayo katika mkutano na wanahabari katika afisi zake za SKM leo.
Alikuwa ameandamana na viongozi kadhaa wa upinzani na waliochaguliwa kupitia chama cha Wiper ambapo alisema, kwamba Maalim ambaye amekuwa akihudumu kama naibu kiongozi ametimuliwa.
Kalonzo alisema kwamba Maalim amekosa kuwa kiongozi wa mabadiliko kama yeye, hata baada ya kumfanyia kampeni huko dadaab wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.
Hatua hii inajiri kufuatia matamshi ya hivi maajuzi ya Farah Maalim katika mkutano uliokuwa na kiongozi wa nchi ambapo alimiminia wakenya matusi akimtetea Rais.
Kalonzo alisema usemi huo ulikiuka kanuni za chama cha wiper.
Mwaka jana, Maalim alitakiwa kufika mbele ya kamati ya nidhamu ya chama cha wiper kufuatia matamshi aliyotoa katika mkutano fulani.
Alisema maneno hayo katika lugha yake asilia na baadaye yalitafsiriwa na ikabainika kwamba alitishia vijana wa taifa hili ambao walifanya maandamano kupinga mswada wa fedha.