Chama cha ODM chatangaza viongozi wapya

Tom Mathinji
1 Min Read
Chama cha ODM chapata viongozi wapya.

Siku chache baada ya manaibu viongozi wa chama cha Orange Democratic Movement ODM kuchaguliwa katika Baraza la Mawaziri, manaibu wapya wa viongozi wa chama hicho wametangazwa leo Ijumaa.

Gavana wa Kisii Simba Arati, mwenzake wa Mombasa  Abdulswamad Nassir pamoja na Seneta wa kaunti ya Vihiga Godfrey Osotsi, wametangazwa na chama hicho kuwa manaibu viongozi.

Katika mabadiliko hayo yaliyotangazwa kupitia ukurasa wa X wa chama cha ODM, Seneta wa kaunti ya Nairobi amedumishwa katika wadhifa huo.

Naye Gavana wa kaunti ya Homa Bay, Gladys Wanga, alivishwa jukumu la mwenyekiti wa chama hicho, wadhifa ulioshikiliwa na waziri wa fedha John Mbadi.

Aidha mbunge wa Rarieda Otiende Amolo na mwenzake wa Turkana Kusini John Ariko, wametangazwa kuwa manaibu wenyekiti wa chama.

Mabadiliko hayo yalifanywa  wakati wa kikao cha Kamati kuu ya usimamizi ya chama hicho iliyoongozwa na kinara wa  chama hicho Raila Odinga.

Viongozi hao wapya wanachukua nafasi zilizoachwa wazi kufuatia uteuzi wa Hassan Joho, Wycliffe Oparanya na John Mbadi katika baraza la mawaziri.

Sifuna alidokeza kuwa kamati kuu ya chama hicho ilipendekeza majina matatu ya watu wanaotarajiwa kuwania wadhifa wa naibu kiongozi wa chama hicho.

Share This Article