Chama cha mchezo wa Raga humu nchini (KRU), kimehairisha michuano yote ya mchezo huo hapa nchini, taifa hili linapoendelea kumuomboleza aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Amollo Odinga.
Kupitia kwa taarifa kwenye ukurasa wake wa X Alhamisi, shirikisho hilo liliagiza vilabu vyote na wahusika wote wa raga kuhairisha mipango yao yote kwa muda wa siku saba za kuomboleza zilizotangazwa na Rais William Ruto siku ya Jumatano.
“Chama cha mchezo wa Raga hapa nchini kinajiunga na nchi kuomboleza na kinatuma rambirambi kwa familia, marafiki na wafuasi wa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga,” kilisema chama hicho.
Chama hicho pia kilisema kinasimama na taifa hili wakati huu mgumu, kikiongeza kuwa shughuli za mchezo wa Raga zitarejelewa baada ya kukamilika kwa kipindi cha maombolezi.
“Tunawashukuru washirika wetu kwa kushirikiana nasi wakati huu mgumu wa majonzi,” iliongeza taarifa ya chama hicho.
Raila Odinga alifariki Jumatano asubuhi, akipokea matibabu nchini India.
Serikali imetangaza siku saba za kumuomboleza Raila, huku bendera zikitakiwa kupeperushwa nusu mlingoti wakati wa kipindi hicho cha maombolezi.