Kulingana na Prof. Lonyangapuo, chama cha KUP kipo katika muungano wa Kenya Kwanza na kwamba hatua ya Pkosing kuanza kukusanya sahihi kumtimua Rais William Ruto madarakani haina maana na ni uamuzi wa kibinafsi.
Wiki jana, Pkosing alisisitiza kuwa ataongoza shughuli ya ukusanyaji sahihi katika ngome ya kisiasa ya Rais Ruto ya North Rift.
Hata hivyo, chama cha KUP sasa kinamtaka Pkosing kujiuzulu wadhifa wake kama mbunge na kutafuta mamlaka upya kutoka kwa raia.
Kulingana na Prof. Lonyagapuo ambaye pia ni Gavana wa zamani wa kaunti ya Pokot Magharibi, chama cha KUP kilitalikiana na muungano wa Azimio punde baada uchaguzi mkuu uliopita na hakina uhusiano wowote na muungano huo.
Alisema KUP kina wabunge watatu ni Pkosing tu peke yake ambaye amekuwa muasi na walimuondoa kama naibu kiongozi wa chama na mahali pake kuchukuliwa na mbunge wa zamani wa Tiaty Asman Kamama.
Mwakilishi Wadi mteule wa UDA Elijah Kasheusheu alielezea mshangao wake na hatua ya Pkosing akisema kaunti ya Pokot Magharibi na ngome ya kisiasa ya UDA.
Aliitaja hatua ya mbunge huyo kuwa ya kisiasa na kumtaka kukoma kutumia jina la Rais Ruto kujinufaisha kisiasa.