Sasa ni rasmi kwamba chama cha kinara wa mawaziri Musalia Mudavadi kitaungana na kile cha UDA kinachoongozwa na Rais William Ruto kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Mchakato wa kuviunganisha vyama hivyo viwili vilivyo katika serikali ya Kenya Kwanza tayari umeanza.
Kumekuwa na tetesi za vyama hivyo viwili kuungana ili kuunda chama kimoja thabiti ila baadhi ya wabunge wa ANC akiwemo mbunge wa Emuhaya walipinga tetesi hizo wakisema ANC haitavunjwa.
Miezi kadhaa baada ya moshi wa tetesi hizo kufuka, sasa Mudavadi ameridhia jitihada za Rais Ruto za kutaka ANC kujiunga na UDA.
Tangazo kuwa chama cha ANC kitajiunga na UDA lilitolewa wakati wa mkutano wa maafisa wa chama hicho uliofanyika katika Ikulu ya Nairobi leo Jumatano.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Mudavadi na kiongozi wa ANC Issa Timmamy ambaye pia ni Gavana wa Lamu.
“Sina mashaka mawazoni mwangu kuwa wazo hilo ni lile ambalo wakati wake umewadia,” alisema Timamy wakati wa mkutano huo.
Kwa upande wake, Mudavadi alisema haitakuwa na mantiki kwa ANC kumsimamisha mgombea wa urais wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Rais Ruto amekuwa mstari wa mbele kupigia debe kuwepo kwa vyama vya kitaifa nchini badala ya vyama vya kikabila.
Alisifia hatua ya ANC akisema itasaidia kukuza mshikamano wa kitaifa.
“Ninadhamiria kuhakikisha kwamba tunabadili siasa za Kenya ili vyama vya kisiasa siku zijazo visiwakilishe mtu binafsi au makabila ila vitambuliwe kwa manifesto, mipango na maono vilivyo nayo kwa nchi,” alisema Rais Ruto.
Haijabainika ni kwa njia gani hatua ya Mudavadi itapokelewa na wafuasi wa ANC hasa magharibi mwa nchi ambayo ni ngome yake ya kisiasa.
Hata hivyo, Mudavadi huonekana kuchukua misimamo inayokinzana na mitazamo ya watu wengi magharibi mwa nchi, ila hatua zake huonekana kuzaa matunda baadaye.
Mfano wa misimamo kama hiyo ni wakati alipoamua kumuunga mkono Rais Ruto wakati wa uchaguzi mkuu uliopita. Ingawa wengi walikosoa hatua yake wakisema ingekuwa bora yeye kujiunga na Azimio, Mudavadi aliishia kuwa katika mrengo ulioshinda urais.
Kutokana na hatua yake ya hivi punde, haijabainika ikiwa chama cha FORD K chake Spika wa bunge la taifa Moses Wetang’ula kitafuata mkondo wa ANC wa kujiunga na UDA kabla uchaguzi mkuu ujao.
Sawia na ANC, viongozi wa FORD Kenya siku zilizopita walipinga vikali jitihada za kutaka chama chao kujiunga na UDA.