CEMASTEA yahitimisha mafunzo ya STEM kwa walimu wa Mandera

Adesh Macan
1 Min Read
Walimu kaunti ya Mandera wapokea mafunzo ya masomo ya STEM

Kituo cha Hisabati, Sayansi, na Elimu ya Teknolojia barani Afrika (CEMASTEA) kimefanikiwa kuhitimisha mpango wa utoaji mafunzo ya siku tano kwa zaidi ya walimu 100 katika kaunti ya Mandera. 

Mpango huo unalenga kuboresha mafunzo ya masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM) kupitia maabara ya mtandaoni.

Mafunzo hayo yaliwalenga walimu wa sekondari ya chini (JS) wanaofunza Hisabati na Sayansi iliyounganishwa kwa wanafunzi wa madarasa ya 7, 8, na 9.

Aidha, mafunzo hayo yaliangazia mtazamo wa kivitendo wa utoaji wa elimu ya STEM, upatikanaji wa maabara ya mtandaoni ya CEMASTEA na utumiaji wa maabara hizo kutoa ushauri na mwongozo wa kitaaluma.

Akizungumzia umuhimu wa mpango huo, Philip Maate kutoka CEMASTEA alielezea imani kuwa mpango huo utafikia malengo yake na kuvutia walimu wengi siku zijazo.

“Tunaamini mafunzo haya yatawatia walimu wengi zaidi moyo wa kukumbatia elimu ya STEM na kufanya utoaji mafunzo katika shule za JS kufanikiwa zaidi,” alisema Maate.

Feisal Kerrow, mwalimu wa kaunti hiyo, aliusifia mpango huo akisema maabara za mtandaoni zitaboresha uelewa wa wanafunzi wa masomo ya STEM.

Adesh Macan
TAGGED:
Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *