Taasisi ya Maendeleo ya Mitaala Nchini, KICD imetakiwa kupunguza idadi ya masomo yanayotolewa chini ya mfumo wa umilisi, CBC.
Wizara ya Elimu nayo imetakiwa kuanzisha matumizi ya mfumo wa Kina wa Shule unaoanzia PP1 hadi Gredi ya 9. Mfumo huo unajumuisha shule ya chekechea, shule ya msingi na shule ya chini, zote zitakazosimamiwa kama taasisi moja.
Imependekezwa matumizi ya neno “sekondari” yafutiliwe mbali kutoka shule ya sekondari ya chini ya sasa na ile ya sekondari ya juu.
Hayo ni baadhi ya mapendekezo ya Jopo la Elimu Lililobuniwa na Rais William Ruto Kuangazia Mageuzi katika Sekta ya Elimu Nchini, PWPER.
Jopo hilo lenye wanachama 53 chini ya uenyekiti wa Prof. Raphael Munavu lilimkabidhi Rais Ruto ripoti yake yenye kurasa 392 katika Ikulu ya Nairobi leo Jumanne.
Katika mapendekezo yake, ripoti hiyo inaitaka KICD kupunguza idadi ya masomo kutoka 9 hadi 7 katika shule ya msingi ya chini, 12 hadi 8 katika shule ya msingi ya juu na 14 hadi 9 katika shule ya chini ili kuwapunguzia walimu na wanafunzi mzigo. Masomo katika shule ya chekechea yamependekezwa kuwa 5 ilhali katika sekondari ya juu kuwa 7.
Jopo hilo kadhalika limeitaka Wizara ya Elimu kufutilia mbali uainishaji wa sasa wa shule za umma kama za kitaifa, shule maalum za kaunti, shule za kaunti na kaunti ndogo na badala yake kutumia uainishaji unaozingatia taaluma wanazopendelea wanafunzi katika shule za sekondari ya juu.
Na ili kuendeleza na kusalia na walimu wenye ujuzi, jopo hilo limependekezwa kutolewa kwa mafunzo ya lazima kwa walimu kwa kipindi cha mwaka mmoja punde baada kuhitimu kabla ya kusajiliwa katika taaluma ya ualimu.
Kulingana na jopo hilo, mfumo wa CBC utaendelea kutekelezwa lakini baada ya kufanyiwa mabadiliko baada ya idadi kubwa ya waliohojiwa kuunga mkono mfumo huo.