Mahakama ya Kimataifa ya Kutatua Migogoro Michezoni (CAS), yenye makao yake mjini Lausane nchini Uswizi imekiri kupokea rasmi rufaa kutoka kwa Shirikisho la Soka nchini Senegal (LSF) linalopinga hatua ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuipokonya timu ya taifa ya Teranga Lions kombe la AFCON.
Kamati ya rufaa ya CAF mnamo tarehe 17 mwezi huu ilitoa uamuzi wa kubatilisha ushindi wa Senegal wa Kombe la AFCON, na badala yake kuipa Morocco ushindi wa mabao 3-0 na kuwatangaza mabingwa.
Hii inafuatia rufaa ya Morocco kwa kamati hiyo kuhusu utovu wa nidhamu wa wachezaji wa Senegal waliotoka uwanjani kuteta penalti waliyopewa kunako dakika za mwisho za fainali ya AFCON Januari 18 mwaka huu.
Jopo la majaji wa CAS litateuliwa na ratiba ya kusikizwa kwa kesi kubainishwa.
Hata hivyo, CAS ilikataa kuelezea muda watakaochukua kusikiza na kutoa uamuzi wa rufaa hiyo.