Cardi B apuuza madai ya Tasha K ya kuwa fukara akitaka amlipe pesa anazomdai

Cardi B aliwasilisha kesi ya kuharibiwa jina na Tasha K mahakamani akashinda na akazawadiwa faini ambayo Tasha anastahili kumlipa. .

Marion Bosire
2 Min Read

Cardi B anataka alipwe pesa anazomdai Tasha K na hakubali madai ya mwanablogu huyo kwamba yeye ni fukara na hana uwezo wa kulipa.

Mwanamuziki huyo anasema ana ushahidi ambao anataka kumpa jaji anayeshughulikia kesi ya ufukara ya Tasha, unaoonyesha kwamba Tasha ana pesa nyingi ambazo amewekeza nje ya nchi kama namna ya kukwepa kumlipa.

Mawakili Cardi waliwasilisha stakabadhi katika mahakama inayoshughulikia kesi za ufukara huko Florida wakimlaumu Tasha kwa deni la dola milioni 3.4 analodaiwa na mteja wao baada ya kushindwa kwenye kesi ya kumharibia jina mwaka 2022.

Tasha alijitangaza kuwa fukara asiyekuwa na mali zozote za kugharamia faini hiyo lakini Cardi anakanusha madai ya ufukara.

kulingana na stakabadhi hizo, Cardi anasema Tasha alibadili umiliki wa mali zake na hata mapato kwa njia ya ulaghai hadi kwa mume wake na kwa jina la biashara yake.

Cardi anasema pia kwamba amegundua akaunti kadhaa za benki nje ya nchi ya Marekani katika maeneo kama the Cook Islands, Nevis na Georgia.

Anadai pia kwamba Tasha anaishi maisha ya kifahari hata baada ya kudai kuwa fukara, akitoa mfano wa nyumba waliyohamia na mume wake ambayo wanalipia kodi ya dola elfu 7, kila mwezi.

Cardi B aliwasilisha kesi ya kuharibiwa jina na Tasha mahakamani baada ya mwanablogu huyo kusema kwenye kipindi chake mara kadhaa kwamba yeye ni changudoa ambaye ni mraibu wa dawa za kulevya na anayeugua magonjwa ya zinaa.

Anamtaka jaji atupilie mbali kesi ya ufukara iliyowasilishwa na Tasha na azuiwe kuwasilisha kesi kama hiyo kwa muda wa miaka miwili.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *