Calin Georgescu aongoza katika uchaguzi wa Urais nchini Romania

BBC
By
BBC
1 Min Read

Mwaniaji urais wa mrengo wa kulia, anayeunga mkono Urusi anaongoza katika awamu ya kwanza ya uchaguzi nchini Romania kulingana na matokeo ya mwanzo.

Huku asilimia 96 ya kura zikiwa zimehesabiwa, Calin Georgescu anaongoza kwa kiwango cha asilimia 22 huku waziri mkuu wa sasa anayeunga mkono Uingereza Marcel Ciolacu akiwa wa pili kwa silimia 20.

Hatua hii imeshtua wengi kwani Georgescu, hana chama na kampeni yake aliiendesha pakubwa kwenye mtandao wa kijamii wa TikTok.

Anaelekea kuwa katika awamu ya pili ya uchaguzi huo pamoja na Ciolacu Disemba 8, 2024.

Georgescu, ameapa kumaliza kile anachokitaja kuwa utiifu kwa muungano wa Ulaya na shirika la kujihami la Nato, hasa katika kuisaidia Ukraine.

Majibu rasmi ya raundi ya kwanza ya uchaguzi huo wa urais nchini Romania yanatarajiwa kutolewa leo Jumatatu.

Kampeni za wawaniaji ziliangazia ongezeko la gharama ya maisha ambapo Romania ina idadi kubwa ya watu walio katika hatari ya kutumbukia katika umaskini katika muungano wa Ulaya.

Wadhifa wa Urais nchini Romania ni jukumu la kiishara tu lakini una ushawishi mkubwa katika masuala kama sera za kigeni.

Idadi ya wapiga kura waliojitokeza kwa uchaguzi huo ni asilimia 51%, kiwango sawia na cha miaka mitano iliyopita.

BBC
+ posts
Share This Article