Shirikisho la kandanda barani Afrika CAF limetangaza kutoa msaada wa shilingi milioni 6.4, kwa kila klabu inayoshiriki mechi za Ligi ya Mabingwa na Kombe la shirikisho kuanzia msimu huu.
Kulingana na Rais wa CAF Dkt. Patrice Motsepe, kila kilabu inayoshiriki michuano ya mchujo ya mataji hayo mawili watapokea hela hizo ili kuwasaidia katika maandalizi.
Mabingwa wa kombe Ligi ya mabingwa watatuzwa shilingi nusu bilioni, huku timu ya pili ikitia kibindoni shilingi milioni 250 ,na kila timu itakayocheza hadi nusu fainali ikipokea shilingi milioni 150.
Timu zitakazocheza hadi kwota fainali zitatuzwa shilingi milioni 116 na milioni 90 kwa timu zitakazomaliza katika nafasi 3 na 4 katika makundi.
Mabingwa wa kombe la shirikisho watabugia shilingi milioni 258 ,huku timu ya pili ikipokea milioni 129.
Vilabu vitakavyocheza hadi nusu fainali vitapokea shilingi milioni 96, na shilingi milioni 70 kwa watakaofika kwota fainali.
Timu zitakazomaliza katika nafasi za 3 na nne katika makundi zitapokea shilingi milioni 51 kila moja .
Hali hii inatarajiwa kuondoa changamoto ambazo zimekuwa kwa timu zinazoshiriki mechi za hatua za mchujo.