Bunge latakiwa kutoa mwelekeo wa kisheria wa kulainisha shughuli za mashirika ya kutatua mizozo

Marion Bosire
2 Min Read

Bunge la kitaifa limehimizwa kuharakisha mchakato wa kisheria wa kuhamisha mashirika yote ya kutatua mizozo hadi kwenye idara ya mahakama.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa miundombinu ya pamoja ya utoaji huduma za mashirika ya utatuzi wa mizozo, tovuti na mwongozo wa usajili, Jaji mkuu Martha Koome aliwataka wabunge waharakishe kupitisha mswada wa mashirika ya kutatua mizozo.

Kulingana naye, kutopitishwa kwa mswada huo kumechelewesha ulainishaji na uendeshaji wa mashirika ya kutatua mizozo nchini.

Wakati huo huo, Koome ameshukuru serikali kwa juhudi zake kuhusu mswada huo hasa kufuatia kuidhinishwa kwake na baraza la mawaziri.

Koome alisema mashirika 26 ya kutatua mizozo yamefanikiwa kuhama kutoka kwenye serikali kuu hadi kwenye idara ya mahakama akisema athari za uhamisho huo tayari zinahisiwa ambapo mashirika hayo yamekuwa yakikamilisha kesi kwa haraka.

Alisema mwaka uliopita wa matumizi ya pesa serikalini, mashirika hayo ya kutatua mizozo yalikamilisha kesi katika kiwango cha asilimia 111, ambapo kesi elfu 15,173 zilikamilishwa ikilinganishwa na elfu 13,712 zilizosajiliwa.

Mashirika ya kutatua mizozo kuhusu kodi, kodi ya nyumba za kibiashara, ushuru na vyama vya ushirika ndiyo yameongoza katika kukamilisha kesi.

Ufanisi huo kulingana na Koome, umethibitishwa pia na kitengo cha kukadiria utendakazi wa mahakama na mashirika ya kutatua mizozo ambacho hufanya tathmini kila mwaka.

Maono ya idara ya mahakama kulingana na Koome ni kuwa na kituo kimoja cha mashirika mbali mbali ya utatuzi wa mizozo ambapo huduma za mashirika hayo zinaweza kutumiwa kwa urahisi.

Alitaja uzinduzi wa miundombinu ya pamoja ya utoaji huduma za mashirika ya utatuzi wa mizozo, tovuti na mwongozo wa usajili kuwa hatua kubwa ya kuhakikisha haki inapatikana kwa urahisi na kuboresha utoaji huduma.

Share This Article