Bunge jana Jumatano lilisitisha ghafla utekelezaji wa mapendekezo ya Jopo la Elimu lililobuniwa na Rais William Ruto Kuangazia Mageuzi katika Sekta ya Elimu Nchini, PWPER.
Jopo hilo lenye wanachama 53 chini ya uenyekiti wa Prof. Raphael Munavu lilimkabidhi Rais Ruto ripoti yake yenye kurasa 392 katika Ikulu ya Nairobi Agosti 1, 2023.
Kulingana na bunge, mapendekezo ya marekebisho katika sekta ya elimu yanahitaji idhini ya bunge kabla ya kutekelezwa.
Hatua hiyo inaleta mkanganyiko mpya katika mtaala mpya wa Elimu ya Umilisi – CBC, huku baadhi ya mapendekezo ya jopo hilo yakiwa tayari yameanza kutekelezwa.
Baadhi ya mapendekezo yaliyokuwa yameanza kutekelezwa ni mfumo mpya wa kutoa alama kwa wanafunzi, mfumo mpya wa kugharimia masomo ya wanafunzi vyuoni, na kuhamishia madarasa ya sekondari ya chini, JS katika shule za msingi.