Bunge lapendekeza kutengwa kwa sehemu kulihusu katika maktaba

Wabunge wanahisi hiyo itakuwa hatua kubwa katika juhudi za kufikisha bunge karibu na wananchi na kupiga jeki mafunzo kuhusu uraia.

Marion Bosire
2 Min Read

Kamati ya bunge la taifa kuhusu utangazaji na maktaba imependekeza kubuniwa kwa sehemu kuhusu bunge katika matawi yote ya maktaba ya kitaifa likiwemo tawi la Mombasa.

Wabunge wanahisi kwamba hiyo itakuwa hatua kubwa katika juhudi za kufikisha bunge karibu na wananchi na kupiga jeki mafunzo kuhusu uraia.

Wanachama wa kamati hiyo walimtembelea Gavana wa Kauni ya Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir, aliyesifia wazo hilo akilitaja kuwa bora na litakalowezesha wananchi kuelewa na kujihusisha na michakato ya bunge.

Walipata fursa ya kuzuru tawi la Mombasa la maktaba ya kitaifa lenye shughuli nyingi wakilisifia kwa jukumu la kuendeleza usambazaji wa elimu ya kujua kusoma na kuandika.

Mwenyekiti wa kamati hiyo ya bunge ya utangazaji na maktaba Daniel Nanok alisisitiza kwamba maktaba zinaweza kuwa vyombo muhimu sana katika kuimarisha demokrasia.

“Maktaba ni vituo vya kuaminika katika jamii. Kwa kuweka sehemu kuhusu bunge humo, wananchi watapata nyaraka na ripoti muhimu za bunge,” alisema Nanok.

Nanok alisema upatikanaji wa nyaraka hizo za bunge utakuza uwajibikaji, elimu ya uraia na ufahamu wa umma.

Kamati hiyo iliahidi kushirikiana na huduma ya kitaifa ya maktaba na serikali za kaunti kuhakikisha utekelezaji wa wazo hilo kote nchini kwa lengo la kufanya bunge kuwa la kupatikana na lenye uwazi kwa wakenya.

Share This Article