Bunge laombwa kupiga marufuku TikTok nchini Kenya

Marion Bosire
2 Min Read

Spika wa bunge la kitaifa Moses Wetang’ula amesema kwamba afisi yake imepokea ombi la kupiga marufuku mtandao wa kijamii TikTok nchini Kenya.

Akizungumza bungeni leo, Wetangula alisema ombi hilo limetoka kwa Bob Ndolo, mkurugenzi mtendaji wa kampuni iitwayo Bridget Connect.

Katika ombi lake, Ndolo anadai kwamba TikTok haifai na inaendeleza lugha isiyo na maadili, vurugu, semi za chuki na picha za ngono.

Kulingana naye TikTok pia inakusanya data za watumiaji wake hasa mahali walipo na historia yao mitandaoni na kisha kutoa habari hizo kwa kampuni nyingine bila idhini.

Anasema iwapo mtandao huo, ambao una uwezo wa kufanya watu kuwa waraibu wake, hautapigwa marufuku, basi utapunguza viwango vya elimu nchini, mbali na kusababisha msongo wa mawazo na ukosefu wa usingizi kati ya watumiaji.

Bob Ndolo anataka bunge liingilie kati na kuokoa wakenya kutokana na mtandao huo.

Hata hivyo kiongozi wa wengi bungeni Kimani Ichung’wa ametetea jukwaa hilo la video akisema hawawezi kupinga teknolojia. Anahisi Ndolo badala yake angeomba bunge lidhibiti matumizi ya TikTok na Wala sio kuipiga marufuku.

Kiongozi wa wachache bungeni Opiyo Wandayi naye alitetea TikTok akisema Kenya haiwezi kujitenga na ulimwengu katika masuala ya teknolojia.

Kuna nchi kadhaa ulimwenguni ambazo zimepiga marufuku TikTok kama vile Afghanistan, Armenia, Azerbaijan na Bangladesh kati ya nyingine barani Asia.

Katika bara Uropa TikTok imepigwa marufuku kwenye nchi kama vile Austria, Belgium, Denmark na Ufaransa kati ya nyingine.

Amerika kaskazini matumizi ya TikTok yamepigwa marufuku nchini Canada kwenye vifaa vya teknolojia vya serikali sawa na nchini Marekani.

Website |  + posts
Share This Article