Bunge la Wawakilishi nchini Marekani kumchunguza Rais Biden

Martin Mwanje
1 Min Read

Bunge la Wawakilishi nchini Marekani litafungua uchunguzi rasmi ili kumuondoa madarakani Rais Joe Biden, mjumbe wake mkuu wa chama cha Republican amesema.

Kevin McCarthy alisema uchunguzi huo utazingatia “tuhuma za matumizi mabaya ya mamlaka, kizuizi na rushwa” dhidi ya Bw Biden.

Warepublican wamekuwa wakimchunguza rais tangu walipochukua udhibiti wa Bunge mnamo Januari.

Vikao hivyo havijapata ushahidi thabiti wa utovu wa nidhamu wa Bw Biden. Hata hivyo, wametoa mwanga zaidi kuhusu shughuli za kibiashara za mtoto wa rais, Hunter Biden, ambazo Warepublican wanasema zinatia shaka na juu ya ufahamu wa Bw Biden kuhusu shughuli za mwanawe.

Katika taarifa yake fupi katika Ikulu ya Marekani, Bw McCarthy alisema kulikuwa na tuhuma “zito na za kuaminika” zinazohusiana na mwenendo wa rais. “Tukijumlisha tuhuma hizi zinatoa taswira ya utamaduni wa rushwa,” alisema.

Ikulu ya White House ililaani uamuzi wa Bw McCarthy. “Wabunge wa Republican wamekuwa wakimchunguza Rais kwa muda wa miezi tisa, na hawajapata ushahidi wowote wa makosa,” msemaji wa Ikulu ya White House Ian Sams aliandika katika chapisho la mtandao wa kijamii.

Share This Article